“JIKWAMUE” YA BENKI YA AZANIA YAWAFAIDISHA WAENDESHA BODABODA KAGONGWA .
Benki ya Azania imezidi kuwafaidisha wajasiliamali wadogo na kuwawezesha kujiongezea kipato baada ya kukabidhi pikipiki mpya 9 kwa waendesha Bodaboda kutoka Kagongwa wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga kupitia mkopo wa masharti nafuu unaotolewa na Benki hiyo maarufu kama “Jikwamue”.
Hafla ya kukabidhi pikipiki hizo imefanyika mwishoni mwa wiki katika tawi la Benki hiyo lililoko Kagongwa, wilayani Kahama na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali akiwamo mbunge wa jimbo la Msalala Mh.Iddy Hamis Iddy, mkuu wa polisi Kagongwa Bw. Oswald Nyarobi, Mchumi wa Halmashauri ya Kahama Bi.Flora Sangilwa, Diwani wa kata ya Kagongwa Bw. Ismail Masolwa pamoja na viongozi wengine wa kata hiyo.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi bodaboda hizo, Meneja wa Benki hiyo tawi la Kagongwa Bw. Prosper Meela alisema kuwa mikopo hii ni mahususi kwa ajili ya makundi mbalimbali ya kijamii ambayo katika masuala ya mikopo huwa yanashindwa kukidhi vigezo na masharti ya kukopesheka, makundi hayo ni kama vile akinamama, vijana, walemavu na makundi maalum. “Kupitia mikopo hii ya Jikwamue, mkopaji atajipatia mkopo bila kuweka dhamana yoyote, atahitaji tu kudhaminiwa na wanakikundi wenzake na kikundi kinaweza kukopeshwa hadi kufikia Shilingi milioni 30 wakati mwanakikundi mmoja anaweza kukopeshwa hadi kufikia Shilingi milioni 3, hivyo walengwa watahitaji kuunda kikundi cha wanachama wasiopungua watano hadi 10 ili kuweza kupata mkopo huu” aliongeza Meela huku akiwaasa wakazi wa eneo hilo kuchangamkia fursa hiyo adimu.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Msalala Mh.Iddy Hamis Iddy aliishukuru Benki ya Azania kwa kutoa mikopo ya aina hiyo ambayo inawasaidia makundi ya vijana ambao wana hamu ya kushiriki katika ujenzi wa taifa lao na kuiomba Benki hiyo iendelee kutoa huduma zenye tija kama hii ya mikopo ya Jikwamue. “Katika kuunga mkono kwa vitendo sera ya Mh Rais John Pombe Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati, ni lazima kuwa na mbinu za kuweza kuwaongezea wajasiliamali na wafanyabiashara wadogo kipato kupitia mashirikiano na Benki zenye misingi imara kama Benki ya Azania ambayo imeonesha ipo tayari kushirikiana na wananchi na serikali katika kufanikisha hilo,’’ alimalizia mbunge huyo.
Naye mkuu wa kituo cha polisi Kagongwa Oswald Nyarobi aliwaasa waendesha bodaboda ambao wamekabidhiwa pikipiki hizo kuwa makini na kutumia pikipiki hizo kwa matumizi yaliyokusudiwa huku wakifuata sheria za matumizi ya vyombo vya moto.
Mikopo hii ya Jikwamue ilizinduliwa mwanzoni mwa mwaka jana ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa Benki hiyo katika kuwainua kiuchumi wajasiliamali wadogo sambamba na kuunga mkono jitihada za serikali ya Mh. Rais John Pombe Magufuli kuinua kipato cha mwananchi kupitia ujasiriamali na biashara ndogondogo.