Benki ya Azania Yazindua Rasmi Tawi lake Dodoma

Benki ya Azania imezidi kujitanua baada ya hii leo kuzindua tawi lake jipya jijini Dodoma ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa benki hiyo katika kukuza mtatandao wa matawi yake sambamba na kuunga mkono jitihada za Mh Rais John Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda, kupitia huduma bora za kibenki.

Akizungumza kwenye hafla ya Uzinduzi wa Tawi hilo ,Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Charles Itembe alisema kwa sasa benki hiyo ina matawi kumi na tisa ikiwemo tawi hilo jipya lilililopewa jina la Sokoine-Dodoma.

“Malengo yetu ya kimkakati kwa sasa ni kukuza mtatandao wa matawi ya benki yetu , angalau matawi matatu kwa mwaka, na pia kukuza nafasi yetu ya umiliki wa soko( Market share) angalau kwa 3% ndani ya miaka mitatu.’’ Alisema Bw Itembe.

Alisema nia ya benki hiyo ni kuwa katika hadhi ya Mabenki Makubwa daraja la kwanza( Tier One ) ndani ya miaka hii mitano ya kimkakati wa kibiashara.

Akizungumzia uamuzi wa kufungua tawi hilo jijini humo, Bw Itembe alisema: “Dodoma ni katikati ya nchi, pili ni makao makuu ya shughuli za kiserikali na pia ni mkoa unaokuwa kwa kasi kibiashara.’’

Aidha, alibainisha kuwa kupandishwa hadhi kwa manispaa ya Dodoma na kuwa jiji kumeiweka benki hiyo katika nafasi nzuri kwa kuwa ukuaji wa jiji hilo unaendana sambamba na mahitaji ya kifedha.

“Katika kuunga mkono sera ya Mh Rais John Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda, ni lazima kuwa na mbinu ya kuweza kukuza kipato kupitia kufanya biashara na benki zenye msingi imara… Azania Benki tupo tayari kushirikiana na wananchi na serikali katika kufanikisha hilo,’’ alisema.

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji mbali na kuipongeza menejimenti ya benki hiyo, aliipa changamoto ya kuhakikisha inaweza kujitanua katika mikoa na wilaya zote za Tanzania Bara na Visiwani na maeneo mengine ndani na nje ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Aidha Dk Kijaji alionyesha kuridhishwa zaidi na namna benki hiyo inavyotoa kipaumbele katika kuboresha sekta ya ujasirimali mdogo na wa kati hatua aliyotaja kuwa itawasaidia makundi hayo kutoa mchango mkubwa katika sekta mbalimbali , ikiwemo ya viwanda vidogo ambayo ndiyo nia ya Serikali ya awamu ya tano.

“Kwasasa serikali inaharakisha utaratibu wa kurasimisha ardhi na kupima viwanja ili wananchi waweze kuwa na dhamana za ardhi iliyopimwa kwa ajili ya kukopesheka kirahisi.’’ Alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Bw Eliud Sanga alisema benki hiyo inaenda vizuri kimikakati na kiutendaji na ndio maana mwaka wa kifedha ulioisha Desemba 2017, ilifunga na faida ya Tsh 1.8 bn/- toka kwenye hasara ya shs. 6 bn/- mwaka uliopita na kuweza kutoa gawiwo la faida kwa wanahisa wake.

Ili kufanikisha shughuli za kibenki hapa nchini hasa katika mkakati wa kujenga uchumi wa viwanda Bw Sanga alishauri masuala kadhaa ikiwemo kuwekeza nguvu ya elimu katika masuala ya fedha pamoja na vigezo vya kupata mikopo kwa wafanyabiashara wadogo na wakati.

“Pia kuendelea na juhudi na kwa kasi nzuri ya kuboresha miundo mbinu kama vile barabara,umeme na huduma nyingine za msingi ili wafanyabiashara hawa waweze kufanya biashara zao kwa gharama ndogo zaidi na mabenki yaweze kuvutika kuwekeza maeneo hayo.’’ Alitaja.

Aidha, Bw Sanga aliishukuru serikali na Benki Kuu kwa kupunguza riba kwa mabenki kwenye kukopa Benki kuu(Discount rates) akitolea mfano mwaka jana ambapo Benki Kuu ilishusha riba kutoka asilimia 16 mpaka asilimia 9 , hatua ambayo imeziwezesha benki kuweza kutoa mikopo kwa riba nafuu.

Mwisho.